Thursday , 16th Jul , 2015

HATIMAYE Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini, kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mh.Joseph Mbilinyi almaarufu Sugu amepata mpinzani aliyetangaza nia leo ya kuwania kiti hicho ndani ya Chama hicho.

Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya Christopher Nyenyembe

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu ya Ubunge katika ofisi za chama hicho wilaya ya Mbeya mjini, Mwandishi wa habari mkongwe na mwakilishi wa kampuni ya magazeti ya Free Media mkoani mbeya,Christopher Nyenyembe amesema endapo atapata ridhaa ya kupeperusha bendera ya CHADEMA atakuwa jirani na wananchi kusikiliza vipaumbele na kuahidi kuvitekeleza kwa asilimia 100.

Nyenyembe ambaye amewahi kuwania nafasi ya Ubunge jimbo la Mbeya mjini katika uchaguzi mkuu mwaka 2010 na kushika nafasi ya tatu kwa tiketi ya CHADEMA akitanguliwa na Mh. Sugu na kufuatiwa na Mponzi ametaja kipaumbele cha pili kuwa ni kuwasemea wanahabari wote mkoani Mbeya.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wakizungumza na kituo hiki kwa nyakati tofauti Hadija Seleman na Anna mwakagile wamempongeza Nyenyembe kwa kuthubutu kwani hiyo ndiyo demokrasia ya kweli ndani ya chama.

Hata hivyo Matron wa kikosi cha Red Brigade cha chama hicho, Agatha Kalonga amesema wanachama wanathamini na kutekeleza kwa vitendo dhana ya demokrasia na hivyo kwa mtia nia huyo kutangaza kuwania nafasi hiyo ni haki yake ya msingi.