Saturday , 15th Jul , 2017

Kocha mtata wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger, amekutana na mshambuliaji wa Monaco, Kylian Mbappe jijini Paris, Ufaransa na kujaribu kumshawishi kujiunga na kikosi chake.

Gazeti la Mirror la Uingereza limeripoti kuwa Wenger, alikutana na mshambuliaji huyo kwa masaa matatu akitumia muda huo kumshawishi kujiunga na Arsenal.

Kocha huyo raia wa Ufaransa amejaribu kumshawishi kinda huyo wa Monaco kwa kumwambia kuwa jiji la London ni sehemu nzuri kwake na Arsenal ni timu sahihi kwake katika kusaka mafanikio zaidi katika soka.

Wenger alijaribu kumshawishi Mbappe kwa kumtolea mfano mkongwe na Arsenal na timu ya taifa ya Ufaransa, Thierry Henry ambaye alijiunga na timu hiyo na kupata mafanikio makubwa.  

Mbappe, pia anawaniwa na klabu nyingine kubwa Ulaya ikiwemo Real Madrid, lakini Wenger amemshawishi kinda huyo kuachana na timu nyingine na kujiunga kwenye kikosi chake ili kupata mafanikio zaidi kama ilivyokuwa kwa Henry.
Wenger anataka kukiimarisha zaidi kikosi chake na wiki iliyopita alikamilisha usajili wa mshambuliaji Alexandre Lacazette.