
Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mama Mary Majaliwa ametoa agizo hilo leo Juni 9, 2018 wakati akifungua Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari Tanzania yanayofanyika kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
"Endapo itabainika yupo mchezaji aliyeletwa kushiriki michezo hii ambaye si mwanafunzi (yaani mamluki) naagiza hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika kwa kuzingatia kanuni na sheria za mashindano haya", amesema Majaliwa.
Pia, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa mikoa na wilaya zote nchini wahakikishe kuwa masomo ya haiba, michezo na stadi za kazi yanafundishwa kikamilifu kwenye shule zote za msingi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaagiza Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe maeneo ya michezo na burudani yanapimwa na yasiingiliwe, pia vitengo vya michezo kwenye ofisi za Halmashauri na Mikoa vitengewe fedha za kuendeshea michezo.