Friday , 29th Apr , 2016

Wazee wa klabu ya Yanga ni kama wameona mbali ama wamesoma alama za nyakati wakati huu klabu hiyo ikiwa katika mbio za ubingwa wa ligi kuu na pia kuwania TFF FA na shirikisho barani Afrika

Mzee Ibrahim Akilimali (kushoto) Katibu wa Baraza la Wazee la klabu ya Yanga.

Baraza la Wazee la Klabu ya Yanga limeiomba Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusogeza mbele muda wa kuanza kwa zoezi la kuchukua na kurejesha fomu za wagombea wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye klabu hiyo.

Hata hivyo baraza hilo halijapinga siku ya kufanyika kwa uchaguzi ambayo ni Juni 5 mwaka huu kamailivyotangazwa na kamati hiyo ya TFF.

Akizungumza leo mjini Dar es Salaam, Katibu wa Baraza la Wazee la klabu hiyo, Ibrahim Akilimali amesema kwamba wanaomba muda usogezwe mbele ili waweze kujiandaa kufanya vizuri katika mechi zilizosalia za Ligi Kuu Bara na mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho.

Akilimali alisema pia Yanga inakabiliwa na mechi muhimu ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola na endapo mchakato wa kuchukua fomu utaanza Mei 4 utawagawa wanachama na kujiweka kwenye mazingira magumu ya kutetea ubingwa na mechi ya Kombe la FA ambayo wataikabili Azam FC.

"Tunaomba mchakazo huu uanze baada ya kumaliza ligi, mechi nne zilizobakia za ligi zinavumilika, vile vile tukiwatoa Waangola tutailetea nchi heshima kwa kufanikiwa kutinga hatua ya makundi," alisema Akilimali.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Aloyce Komba aliliambia gazeti hili jana kwamba kalenda iliyotangazwa na kamati yake haitabadilika na kuwataka wanachama wa Yanga kujiandaa na uchaguzi huo.

Wakili Komba aliwataka wanachama wa Yanga kuwaacha viongozi na watendaji wa kila siku wa klabu kuendelea kuisimamia timu yao na leo kamati yake itakutana ili kukamilisha taratibu za uchaguzi huo.

Viongozi wa Yanga walioko madarakani walimaliza muda wao wa kuongoza klabu hiyo kwa mujibu wa katiba tangu mwaka juzi.

Kamati hiyo ya TFF ilitangaza uchaguzi huo wa Yanga baada ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuitaka klabu hiyo kufanya uchaguzi wake kabla ya Juni 30 kufuatia uongozi ulioko madarakani kutotambulika kisheria.

BMT pia ilitoa mwongozo kuwa katiba itakayotumika katika uchaguzi huo ni ya mwaka 2010 na kutoitambua katiba mpya iliyofanyiwa marekebisho 2014.