Wednesday , 3rd Jun , 2015

Wanariadha watatu wa Tanzania walioweka kambi katika kituo cha kimataifa cha Kip Keino High Altitude Training Centre cha Eldoret nchini Kenya wamesema kambi hiyo itawasaidia kufunika rekodi za wanariadha wanaoshikilia rekodi za Dunia.

Katika taarifa zao kwa nyakati tofauti, wakiwa nchini humo, wanariadha hao wamesema, katika kambi hiyo hakuna mwanariadha yoyote maarufu na mazoezi wanayopewa yanalenga kuhakikisha miongoni mwao wanapatikana wanariadha watakaoleta mapinduzi kwa wanariadha maarufu Duniani.

Kwa muda sasa wanariadha hao wapo kambini nchini humo kwa ajili ya kujiandaa na michezo ya Olimpiki Rio 2016.

Wanariadha hao ambao ni Fabian Sulle, Bazil Baynit na Fabian Naas wameungana na wanariadha kutoka katika mataifa mbalimbali ya Afrika kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya mazoezi ya kujiandaa na michezo ya Olimpiki Rio 2016 chini ya Programu ya Olimpiki Solidarity ya kuwaandaa vijana wanaotarajiwa kuwa mabingwa.