Saint Louis Suns United ambayo ilitua nchini tangu Alhamisi, ni klabu inayotokea katika jiji la Victoria, nchini Shelisheli. Timu hiyo iliundwa mwaka 2007 kwa kuunganisha vilabu viwili vya Saint-Louis iliyoanzishwa mwaka 1985 na Sunshine iliyoanzishwa mwaka 1993.
Saint Louis kabla ya kuungana na Sunshine ilikuwa imetwaa ubingwa wa ligi kuu ya Shelisheli mara 13 kati ya miaka ya 1979 na 1994. Sunshine ilikuwa imetwaa mara moja ambayo ni mwaka 1995.
Saint Louis Suns United imekuwa ikishiriki michuano hii ya CAF kwa misimu kadhaa ambapo mara zote imekuwa ikiondolewa katika hatua za awali isipokuwa mwaka 2001 ilipokuwa ikitambulika kama Saint-Louis ambapo ilifika raundi ya pili ya michuano hiyo.
Yanga inahitaji ushindi katika mchezo wa leo ili kujiweka vyema katika mchezo wa marejeano utakaopigwa wiki mbili zijazo huko Victoria Shelisheli. Yanga imeongezewa nguvu na urejeo wa nyota wake kama Ibrahim Ajib, Youthe Rostand na wengine ambao walikuwa majeruhi.


