Kushoto ni Baraka Sadick wa Mchenga Bball Stars na kulia ni Baraka Mopele wa Flying Dribblers.
Kuna vitu mbalimbali vya kuvutia kwenye fainali hizo ambapo vita ya pointi inaonekana kuwa kivutio namba moja ikiwa hadi sasa mchezaji Baraka Sadick wa Mchenga Bball Stars anaongoza kwa kufunga pointi nyingi katika tyimu hizi mbili zilizoingia fainali akiwa na jumla ya pointi 100.
Anaye mfuatia kwa karibu ni Baraka Mopele kutoka timu ya Flying Dribblers ambaye mpaka sasa kafunga pointi 92, hivyo wawili hawa watakuwa wanaziongoza timu zao kuelekea kuzipata zile milioni 10 kwa bingwa, milioni 3 kwa mshindi wa pili na kubwa zaidi kwao kama wachezaji ni ile zawadi ya mchezaji bora yaani 'MVP' ambayo ni milioni 2.
Mbali na hilo timu zote zimefanya mabadaliko ya wachezaji ambao walishiriki msimu uliopita, wengine wakiwepo na wengine hawapo. Kwa upande wa Mchenga Bball Stars wao wameongeza sura mpya lakini wengi wamebaki walewale ila wanamkosa Rwehabura Munyagi ambaye ndio alikuwa MVP wa mashindano mwaka 2017.
Kikosi chao cha msimu huu kina nyota kama Baraka sadick, Cristian Joseph, Jije Makani, Mgosi Nyameta, Johnson Mohamed, Mohamed Yusuf, Cornelius Mgaza, Ivan Tarimo, Amos Christian na Masero Nyirabu.
Kwa upande wa Flying wao pia wamefanya mabadiliko lakini kikosi chao kimebaki na asilimia kubwa ya wachezaji waliokuwepo msimu uliopita. Mchezaji ambaye wanamkosa uwanjani ni Geofrey Lea lakini wapo naye kwa upande mwingine akiwa kama kocha msaidizi.
Kikosi chao kamili kina wachezaji kama Habirmana Mayeye, Baraka Mopele, Shenta Denis, Elias Samwel, Benedict Kafuru, Mussa Hassan, Steve Mtemihonda, Meddy Makani, Hermes Lazaro na John Mashauri.