Tuesday , 6th Dec , 2016

Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) imesema miongoni mwa mambo itakayoyaangalia kwa umakini mkubwa katika mzunguko wa pili wa ligi ni waamuzi, ili kuhakikisha wanatenda haki na kuondoa malalamiko yaliyoshamiri katika mzunguko wa kwanza.

Boniface Wambura - Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi

 

Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo , Boniface Wambura amesema maandalizi ya mzunguko huo yanaendelea vizui na kamati ya waamuzi tayari imeanza vikao vyake kuanzia jana kwa ajili ya kupanga ratiba ya waamuzi pamoja na kutathmini yaliyojiri katika mzunguko wa Kwanza.

Amesema maandalizi mengine yanayoangaliwa hivi sasa ni viwanja vyenye mapungufu ambapo bodi hiyo imevitaka vilabu vyote ambavyo viwanja vyao vina mapungufu watoe taarifa sasa kwa ajili ya marekebisho pamoja na kuvihakiki kabla ligi haijarejea.

Wambura pia amesisitiza kuwa tarehe ya kuanza kwa mzunguko huo iko palepale ambayo ni Desemba 17, na kwamba hivi sasa dirisha dogo la usajili linaendela na litafungwa mnamo Desemba 15 huku akieleza imani yake kuwa mzunguko wa pili utakuwa ni wenye ushindani zaidi.