
Simba na Yanga, mazoezini
Akiongea na www.eatv.tv msemaji wa Ruvu Shooting Masau Bwire amesema mechi zao zote zijazo dhidi ya Simba na Yanga hazitachezwa kwenye uwanja wa taifa kama ilivyojulikana badala yake watazipeleka uwanja wa Jamhuri Dodoma.
''Mechi zetu dhidi ya timu hizi zimekuwa zikichezwa taifa hata kama tupo nyumbani hivyo tumefikiria vizuri na kuzingatia maombi ya mashabiki wetu mikoani tumefikia maamuzi ya kupeleka mechi hizo kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma'', amesema.
Bwire amesisitiza kuwa tayari wameshawasiliana na Bodi ya ligi kuwajulisha nia yao hiyo ya kutumia uwanja wa Jamhuri Dodoma katika mchezo wa marudiano na Yanga ikizingaia tayari mchezo wa kwanza dhidi ya Simba umeshachezwa taifa na Ruvu Shooting walikuwa wenyeji hivyo itawalazimu kurudi tena taifa kucheza na Simba wakiwa kama wageni.
Ruvu Shooting imekuwa timu ya pili kuondoa mechi zake za nyumbani kwenye uwanja wa Taifa baada ya JKT Tanzania nayo kuhamia uwanja wa Mkwakwani Tanga kwaajili ya mechi za Simba na Yanga.
Bwire amesema kulikuwa na maombi ya mikoa mbalimbali kuwa wenyeji wa mechi hizo lakini wameamua kuichagua Dodoma kwa kuwa tayari ni makao makuu rasmi ya taifa na hakuna timu ya ligi kuu hivyo watakuwa na mashabiki wengi.