Tuesday , 7th Apr , 2015

Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya soka Afrika Mashariki Na Kati CECAFA, Leodgar Tenga amerejea katika nafasi yake ya Ujumbe wa kamati ya utendaji ya shirikisho la Soka Afrika CAF baada ya uchaguzi uliokwenda sambamba na mkutano Mkuu.

Tenga, Rais wa zamani wa Shirikisho La Soka Nchini TFF, sasa ataitumikia nafasi hiyo kwa miaka mingine minne kama mkuu wa Ukanda wa CECAFA.

Taarifa kutoka kwa katibu Mkuu wa CECAFA, Nichola Musonye imesema mkutano mkuu wa CAF ambao hufanyika kila mwaka ulianza Aprili sita mpaka saba mwaka huu mjini Cairo, Misri na nchi zote 54 wanachama zikiwemo 12 za CECAFA zilihudhuria.

Wanachama wa CECAFA ni Burundi, Kenyam Uganda, Tanzania, Somalia, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Zanzibar, Rwanda, Sudan na Sudan Kusini.

Tenga alichaguliwa bila kipingamizi baada ya aliyekuwa mpinzani wake, Hassan Suleiman wa Djibout kujitoa na kumsapoti nahodha huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.