Sunday , 11th Nov , 2018

Baada ya kiungo mshambuliaji wa Simba raia wa Zambia, Clatous Chama kuwika klabuni hapo katika mechi za karibuni, hatimaye Haruna Niyonzima ameibuka na kutoa kauli yake juu ya mchezaji huyo.

Haruna Niyonzima (kushoto) na Clatous Chama (kulia)

Niyonzima ambaye anacheza nafasi sawa na mchezaji huyo amekiri kwamba kiungo mwenzake, Clatous Chama anaujua mpira vizuri lakini anamzidi uwanjani kwa sababu yeye ni mwepesi kuliko Mzambia huyo.

Katika mechi za hivi karibuni, Clatous Chama aliyesajiliwa kutokea Power Dynamos ya kwao Zambia amecheza kwa kiwango kikubwa kiasi cha kuwavutia mashabiki wa Simba na kumsahau kabisa Niyonzima ambaye hajaonekana kwa muda mrefu uwanjani tangu aliposajiliwa na Simba msimu uliopita.

Niyonzima amesema yeye na Chama ni marafiki wakubwa na wamekuwa wakizungumza vizuri tofauti na wengi wanavyodhani yeye yuko juu zaidi ya Mzambia huyo kwa sababu mambo anayoyafanya uwanjani anafanya kwa taratibu tofauti na yeye ambaye anafanya kwa uharaka.

Chama ni kiungo mzuri sana na anaujua mpira, mara nyingi tumekuwa tukizungumza vizuri kuhusiana na masuala ya uwanjani tofauti na watu wanavyoona kwamba eti sisi ni maadui," amesema.

Hatufanani kiuchezaji kwa sababu yeye vile vitu anavyofanya uwanjani anafanya kwa uzito fulani hivi tofauti kabisa na mimi ambaye ninafanya hivyohivyo lakini kwa uharaka zaidi, hivyo hatuwezi kuwa sawa hata kidogo,” ameongeza Niyonzima.