Sunday , 3rd Aug , 2014

Ule usemi unaosemwa sikio la kufa halisikii dawa ama mwenye nacho anaongezewa umetimia wikii hii baada ya timu za soka za taifa za Tanzania Taifa Stars na ya vijana Serengeti Boys kutupwa nje katika michuano ya kusaka tiketi ya michuano ya Afrika

Kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania taifa stars

Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars imevurumishwa nje ya michuano ya kusaka tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika AFCON 2015 baada ya hii leo kuchabangwa magoli 2-1 na The Mambaz ya Msumbiji, katika mchezo wa marudiano uliopigwa Maputo nchini humo.

Ikumbukwe katika mechi ya kwanza iliyochezwa jijini Dar es Salaam Majuma mawili yaliyopita timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. na kwa ushindi huo wa jumla wa mabao 4-3 sasa msumbiji imeingia kwenye kundi lenye timu za Cape Verde,Niger na Zambia katika hatua ya makundi na mshindi wa kundi hilo ataungana na washindi wengine katika ngarambe ya fainali hizo zitakazopigwa nchini Morocco mwakani

Mzimu ama mdudu wa nuksi katika soka nchini ulianza hapo jana baada ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kuaga michuano ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa vijana zitakazofanyika mwakani nchini Niger baada ya kufungwa magoli 4-0 na timu ya Afrika Kusini (Amajimbos) katika Mechi ya marudiano ya raundi ya pili iliyochezwa hapo jana kwenye Uwanja wa Dobsonville uliopo Soweto nchini humo,

Serengeti Boys iliyo chini ya kocha mzalendo Hababuu Ally Omar ilihitaji sare ya idadi yoyote ya magoli ama ushindi wa aina yoyote ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele lakini hali ilikuwa tete na kuwaacha vijana wa Hayati Madiba wakisonga mbele kwa ushindi huo mzito wa mabao 4-0 ambapo katika mchezo wa awali timu hizo zilitoka sare tasa jijini Dar es salaam katika dimba la Azam complex chamazi.