Wednesday , 6th Apr , 2016

Katika kuonyesha kuwa suala la nidhamu ni jambo la kwanza kwa klabu ya soka ya Simba baada ya kumwadhibu beki Hassan Isihaka na kumlima barua kiungo Abdu Banda klabu hiyo imewageukia wachelewaji wawili Hamis Kiiza na beki kisiki Jurko Murshid.

Mshambuliaji wa Simba Hamis Kiiza ambaye ni kinara wa mabao ligi kuu kwa sasa.

Wachezaji wawili wa kimataifa wa Simba kutoka Uganda, mshambuliaji Hamisi Kiiza na beki kisiki Juuko Murshid, huenda wakakumbana na adhabu ya kusimamishwa kutokana na kuchelewa kurejea nchini kuungana na timu hiyo inayoongoza kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara.

Uongozi wa Klabu ya Simba umesema straika wao, Hamisi Kiiza na beki wa timu hiyo, Juuko Murshid, watatakiwa kuandika barua za kujieleza kutokana na kuchelewa kujiunga na wenzao ambao wapo katika maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

Tangu wachezaji hao raia wa Uganda waondoke nchini wiki mbili zilizopita kwenda kuitumikia timu yao ya taifa katika michezo ya kufuzu Michuano ya Mataifa Afrika (Afcon 2017) dhidi ya Burkinafaso, mpaka leo bado hawajarejea huku kukiwa hakuna taarifa zozote zinazoeleza juu ya kuchelewa kwao.

Mkuu wa Idara ya Habari wa Simba Haji Manara, amesema uongozi wa klabu hiyo umepanga kuwandikia barua ya kujieleza na kutolea ufafanuzi wa kile kilichowafanya kuchelewa kurudi kujiunga na wenzao.

Kiiza ndiye anayeongoza kwa kupachika mabao msimu huu akiwa amefikisha magoli 19 akifuatiwa na Amissi Tambwe wa Yanga aliyecheka na nyavu mara 18.

Katika hatua nyingine, Manara amesema sakata la beki wao, Abdi Banda limepelekwa katika Kamati ya Nidhamu ya Simba na huko ndipo watatoa hukumu ya kesi yake.

Banda kwa sasa amesimamishwa na Simba kwa kile kilichoelezwa kumgomea kocha wake, Jackson Mayanja alipomtaka apashe misuli ili aingie uwanjani kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Coastal Union uliopigwa Machi 19 mwaka huu katika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.