Evance Aveva rais wa Klabu ya Simba
Baada ya kilio cha muda mrefu cha wanachama wa klabu ya soka ya Simba kutaka kupatikane njia mbadala ya kuinusuru klabu yao na kuiwezesha kiuchumi ili iweze kushindana na vilabu vingine vikubwa nchini na nje hii leo ungozi wa klabu ya Simba umesikia kilio cha wanachama hao.
Usikivu huo unatokana na kitendo cha rais wa timu hiyo Evans Aveva kutangaza kuunda kikosi kazi ama kamati maalumu ya watu wanne itakayoratibu zoezi la kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo ili iweze kujinusuru kutoka hapa ilipo na kupiga hatua mbele zaidi.
Aveva ameunda kamati hiyo ya watu wanne itakayoongozwa na Alhaj Aziz Kefile akisaidiwa na Ally Suru pamoja na wajumbe wengine wawili ambao wamepewa mwezi mmoja kukamilisha jukumu hilo zito la kuandaa mapendekezo ya mfumo gani utumike kwaajili ya kuiendesha klabu hiyo kisasa na kuinusuru katika mapito inayopita sasa na kuwa klabu isiyo na ushindani.
Aidha, Aveva amesema baada ya siku hizo 30 kamati hiyo itawasilisha mapendekezo hayo kwa kamati ya utendaji ya klabu hiyo ambayo baaada ya kuyapitia itawasiliasha kwenye mkutano wa wanachama ambao ndiyo wenye mamaka ya kufanya maamuzi ya mwisho kikatiba na kuamua ni mfumo gani utafaa kuiendesha klabu hiyo kwa mafanikio kwa mujibu wa mapendekezo ya kamati hiyo ya kuratibu mfumo upi unafaa kuiendesha klabu hiyo kimaendeleo hasa katika kujikwamua kiuchumi.
Wakati huo huo Uongozi wa klabu hiyo umewaomba radhi wanachama na mashabiki wao kutokana na matokeo mabovu ya timu yao msimu huu na kupelekea timu hiyo kukosa kwa mara nyingine uwakilishi wa kimataifa kwa msimu wa nne sasa.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa klabu hiyo Evans Aveva wakati akizungumza na wanahabari kuhusiana na sababu za timu hiyo kuboronga ambapo ametoa sababu nyingi ikiwemo uwepo wa wachezaji mamluki akiwaita wasaliti lakini pia akalitupia lawama shirikisho la soka nchini TFF.
Aveva amesema baadhi ya wachezaji wa timu hiyo walikua wakifanya matendo ya utovu wa nidhamu kwa makusudi ama kwa kupanga na watu wasioitakia mema timu hiyo akiwataja kuwa ni wapinzani wa timu hiyo.
Aveva amewataja wachezaji hao kama wasaliti kutokana na matukio yao ya utovu wa nidhamu kwa wakuu na viongozi wa benchi la ufundi wa klabu na pia kufanya matendo ya kiutovu wa nidhamu viwanjani wakati wa mchezo na kutolewa nje kwa kadi nyekundu adhabu ambazo ziliigharimu timu hiyo na akatoplea mfano mchezaji anapewa adhabu na klabu kisha unamsikia amejiunga na klabu inayotuhumiwa kumtumia mchezaji huyo kufanya hujuma na wengine kutumika kuhamasisha migomo isiyo na tija kwa klabu.
Aveva amesema suala lingine ni waamuzi, na mabadiliko ya ratiba imekuwa ni moja ya sababu zilizochangia kiasi kikubwa kuidhoofisha na kuathili mwenendo wa timu hiyo hasa ikichangiwa kwa kiasi kikubwa na Shirikisho la Soka nchini Tanzania TFF ambao wamekuwa wakichelewa kutoa maamuzi ya masuala mbalimbali ya kikanuni lakini pia maamuzi yakitolewa yanaegemea upande ambao unamaslai yao.
Akimalizia Aveva amesema kwa mfumo huu wa kuendesha mpira wa mslahi ya wachache basi ni vigumu kupata wawakilishi bora wa michuano ya kimataifa kama ilivyokuwa zamani na hivyo kujikuta kila mara tukiishia hatua za awali na kubakia kujivunia rekodi za miaka ya nyuma.