Friday , 17th Jun , 2016

Uongozi wa klabu ya Simba umefanya mazungumzo na kocha Sellas Tetteh Teivi, raia wa Ghana ambaye ni mmoja wa makocha maarufu barani Afrika.

Kwa sasa kocha huyo gwiji barani Afrika, ndiye kocha mkuu wa timu ya taifa ya Sierra Leone na Simba imefanya mazungumzo naye kwa takribani wiki nzima.

Klabu hiyo tayari imetenga dau kwa ajili ya kocha huyo na kinasubiriwa ni yeye kusema ndiyo.

Kocha huyo aliyewahi kuinoa timu ya taifa ya Ghana, ni maarufu kutokana na mambo kadhaa likiwemo lile la kuiongoza timu ya vijana wa Ghana chini ya miaka 23 kucheza Kombe la Dunia mwaka 2013.

Pia aliwahi kuwa kocha wa muda wa timu kubwa ya taifa ya Ghana na wakati akiwa mwanasoka, alicheza kwa mafanikio katika klabu za Great Mao Mao, Zebi na Hearts of Oak kwao Ghana, pia nchini Nigeria alipozitumikia ACB, Julius Bereger na Iwuanyanwu.