Mchezaji wa Simba SC Ibrahim Ajib akiwa amembeba Hamisi Kiiza wakishangilia moja ya magoli yao kwenye mchezo dhidi ya Mgambo JKT
Kwa mabao hayo, Simba SC imefikisha pointi 39 baada ya kucheza mechi 17, sasa ikiwa inazidiwa pointi moja tu na mabingwa watetezi, Yanga SC walio kileleni, wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 39 pia.
Mshambuliaji Mganda, Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliifungia Simba SC bao la kwanza dakika ya tano akimalizia krosi ya mshambuliaji Ibrahim Hajib.
Kiiza akakosa penalti dakika ya 14 iliyookolewa na kipa Mudathir Khamis, kufuatia Henry Chacha kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
Dakika ya 28 Mwinyi Kazimoto akafunga bao la pili kwa shuti kali kutoka nje ya boksi baada ya kugongeana vizuri na Hajib.
Hajib akaenda kufunga mwenyewe bao la tatu dakika ya 42 baada ya kuwachambua mabeki watatu wa Mgambo na kipa wao Mudathir Khamis, kufuatia pasi ya Kazimoto.
Daniel Lyanga aliyetokea benchi kuchukua nafasi ya Hajib kipindi cha pili, aliifungia Simba SC bao la nne kwa shuti kali kutoka nje ya boksi baada ya pasi ya kiungo Said Ndemla.
Kiiza akahitimisha karamu ya mabao ya Simba SC kwa kufunga bao la tano dakika ya 82 akimalizia krosi ya Hassan Kessy huku Fully Maganga akiipatia Mgambo bao la kufutia machozi dakika ya 88 baada ya mabeki wa Simba SC kumuacha wakidhani ameotea.
Kwa upande wa Yanga SC imezidi kupoteza matumaini ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya baada kulazimishwa sare ya 2-2 na Prisons Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Matokeo hayo hayaiondoi kileleni Yanga SC ikifikisha pointi 40 baada ya kucheza mechi 17, mbele ya Azam FC na Simba SC wenye pointi 39 kila mmoja lakini Azam FC wana viporo wawili, wakati Simba SC ndiyo wamecheza mechi 17 kama Yanga.
Yanga SC walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji wake Mrundi, Amissi Tambwe aliyefunga kwa kichwa akimalizia krosi ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima.
Prisons wakasawazisha bao hilo kupitia kwa Jeremiah Juma aliyefunga kwa kichwa pia dakika ya 40 akimalizia krosi ya Mohammed Mkopi.
Mkopi akaifungia Prisons bao la pili dakika ya 62 kwa kichwa pia akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo wa zamani wa Yanga SC, Juma Seif ‘Kijiko’.
Dakika ya 84 ya mchezo Simon Msuva aliyetokea benchi kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Deus Kaseke aliisawazishia Yanga kwa baada ya beki Meshak Suleiman kuunawa mpira kwenye boksi.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Vincent Angban, Kessy Ramadhani, Abdi Banda, Juuko Murshid, Hassan Isihaka, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamisi Kiiza, Ibrahim Hajib/Danny Lyanga dk72 na Hija Ugando/Said Ndemla dk62.
Mgambo JKT; Mudathir Khamis, Bakari Mtama/Bolly Shaibu dk44, Salim Mlima, Salim Kipaga, Ramadhani Malima/Mussa Ngunda dk44, Henry Chacha, Sunday Magoja, Mohammed Samatta, Fully Maganga, Ally Nassor na Aziz Gilla.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Said Juma ‘Makapu’/Salum Telela dk59, Deus Kaseke/Simon Msuva dk54, Haruna Niyonzima na Donald Ngoma, Amissi Tambwe na Issoufou Boubacar.
Prisons; Benno Kakolanya, Benjami Asukile, Laurian Mpalile, James Mwasota, Nurdin Chona, Jumanne Fadhil, Lambert Sadianka, Freddy Chudu/Juma Seif dk48, Mohammed Mkopi, Jeremiah Juma na Leonce Mutalemwa/Meshack Suleiman dk51.
Matokeo ya mechi zote zilizochezwa leo:
Mtibwa Sugar 2-2 Toto Africans
African Sports 1-0 Mwadui FC
Kagera Sugar 2-1 Majimaji
Simba SC 5-1 Mgambo JKT
Tanzania Prisons 2-2 Yanga


