Saturday , 13th Feb , 2016

Klabu ya Simba SC inatarajiwa kwenda Morogoro hapo kesho kuweka kambi kwa ajili ya mchezo wa marudiano wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao Yanga SC utakaofanyika Jumamosi ijayo uwanja wa Taifa, Dar es salaam.

Simba SC itatua Moro 'Mji Kasoro Bahari' kesho ikitokea mkoani Shinyanga ambako leo itamenyana na Stand United katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu na hiyo ni tofauti na mazoea ya klabu kuweka kambi Zanzibar kabla ya mchezo wa mahasimu wao hao.

Yanga SC ambayo ipo Mauritius ambako leo watamenyana na Cercle de Joachim SC baada ya mchezo watapanda ndege kwenda kuweka kambi kisiwani Pemba.

Ikumbukwe mechi ya mzunguko wa kwanza Simba ililala 2-0 mabao ya Malimi Busungu na Amissi Tambwe.

Hata hivyo, Februari 20, Simba SC wataingia uwanja wa Taifa na kocha mwingine, Mganda Jackson Mayanja aliyeichukua timu mwezi uliopita baada ya kufukuzwa muingereza, Dylan Kerr ambaye Yanga ilimfunga 2-0 mwaka jana.