Tuesday , 23rd Dec , 2014

Klabu ya Simba ya jijini Dar es salaam, imeahidi kujivunia pointi tatu muhimu katika mechi yake dhidi ya Kagera Sugar inayotarajiwa kuchezwa Desemba 26 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.

Akizungumza na East Africa Radio, Afisa Habari wa Klabu hiyo, Humphrey Nyasio amesema anaamini usajili pamoja na juhudi za mazoezi kwa wachezaji wa klabu hiyo, vitasaidia kuweza kuibuka na ushindi katika mechi zote za ligi zilizobakia.

Nyasio amesema timu inaendelea na mazoezi visiwani Zanzibar ambapo inatarajiwa kurudi Alhamisi ya Desemba 25 kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo.

Nyasio amesema wachezaji ambao hawakuwa kambini tayari wameshawasili kambini kujiunga na kikosi hicho kwa ajili ya kuendelea na mazoezi isipo kuwa mchezaji Emmanuel Okwi ambaye anatarajiwa kuwasili nchini akitokea Uganda hapo kesho ambapo atasubiri kikosi kitakapowasili ndipo atajiunga nacho.

Nyasio amesema hati za Uhamisho wa Kimataifa ITC za wachezaji wa timu hiyo zimeshakamilika na kilichobakia ni vibali vya kazi ambavyo vinaendelea kushughulikiwa na klabu hiyo.