
Mapema leo asubuhi kikosi cha Simba kimefanya mazoezi ya Gym kwenye Gym ya Police Academy jijini Dar es Salaam. Mbali na mazoezi hayo ya Gym lakini kikosi hicho pia jana kilifanya mazoezi ya Stamina kwenye ufukwe wa Coco jijini Dar es salaam.
Programu hizo za mazoezi bado zinasimamiwa na kocha msaidizi wa timu hiyo Masoud Juma. Kocha mkuu Joseph Omog bado hajarejea nchini kutoka kwao Cameroon lakini hivi karibuni klabu ilithibitisha kuwa atarejea ndani ya wiki hii.
Jioni hii Simba imeendelea na mazoezi katika viwanja vya Polisi jijini Dar es Salaam ikiwa na kikosi chake cha wachezaji ambao hawakujumuishwa kwenye timu za taifa kwaajili ya CECAFA. Lakini mchezaji Said Hamis Ndemla ameongeza nguvu baada ya kurejea kutoka kwenye majaribio yake nchini Sweden.
Simba inaongoza ligi ikiwa na alama 23 sawa na Azam FC yenye alama 23 zikitofautiana magoli ya kufunga na kufungwa. Kikosi hicho kinajiandaa na mchezo wa raundi ya 12 ligi kuu soka Tanzania Bara dhidi ya Ndanda FC.