Wednesday , 14th Jan , 2015

Simba SC imefanikiwa kuibuka mabingwa wa Kombe la Mapinduzi kwa mara ya tatu baada ya kuifunga Mtibwa Sugar kwa Penati 4-3 kufuatia kutoka sare ya 0-0 katika dakika 90 za mchezo, mechi iliyochezwa uwanja wa Amani, Zanzibar.

Mchezo huo ulianza huku kukiwa na ushindani Mkubwa kutokana na kila timu kuhitaji kupata ushindi ili kuweza kuibuka Mshindi wa Michuano hiyo.

IVO MAPUNDA ndiye aliyeibuka shujaa wa mchezo huo baada ya kupangua penati ya mwisho ya Vicent Barnabas wa Mtibwa Sugar huku penati nyingine ikigonga mwamba.

Penati nne simba zimefungwa na Awadhi Juma, Kessi Ramadhan, Hassan Isihaka, na Dan Sserunkuma wakati Shaban Kisiga akikosa penati moja.

Penati tatu za Mtibwa Sugar zimefungwa na Ally Lundenga, Shaban Nditi na Kichuya Ramadhan, wakati Ibrahim Jeba na Vicent Barnabas wakikosa penati zao.

Kombe hilo limetolewa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, ambapo amemtaka Kipa aliyeidakia timu ya Simba kwa Dakika 90 kabla ya kumpisha Ivo Mapunda kudaka mikwaju ya Penati, Peter Manyika kuongeza juhudi zaidi ya hapo na kuwa bora zaidi hapo baadaye.