Wednesday , 25th Jan , 2017

Klabu ya Simba huenda ikatupwa nje ya michuano ya kombe la shirikisho kufuatia kumpanga beki wake Novalt Lufunga kwenye mchezo walioshinda mabao 2-0 dhidi ya Polisi ya Dar es salaam huku akiwa na kadi nyekundu aliyoipata kwenye michuano iliyopita.

Mchezo kati ya Simba na Polisi Dar

Kwa mujibu wa rufaa ya klabu ya Polisi inadai kwamba Lufunga alilimwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa mwisho wa michuano hiyo msimu uliopita dhidi ya Coastal Union ya Tanga ambapo Simba ilitupwa nje ya mashindano.

Shirikisho la Soka nchini TFF limesema, malalamiko ya timu ya Poilisi ya Dar es salaam juu ya Simba SC kumchezesha mchezaji Novart Lufunga aliyekuwa na adhabu ya kadi nyekundu katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Tanzania Bara lyamefika na yatafanyiwa kazi kwa mujibu wa sheria za soka.

Afisa habari wa TFF Alfred Lucas amesema, suala hilo lilifikishwa katika kamati ya saa 72 ya TFF likielezea kuwa Lufunga alipata kadi nyekundu katika mchezo wa FA msimu uliopita dhidi ya Coastal Union ya jijini Tanga hivyo suala hilo linashughulikiwa mapema kabla ya kuendelea kwa Ligi hiyo katika hatua ya 16 bora ambayo inatarajiwa kuendelea Mwezi Februari mwaka huu.

EATV imezungumza na Makamu wa Rais wa Klabu ya Simba Geofrey Nyange 'Kaburu' ambaye amelitolea ufafanuzi suala hilo huku akikanusha kuwa Lufunga hakucheza mchezo uliofuata baada ya ule wa Coastal, lakini pia akasema kuwa kanuni za mashindano hayo ni tofauti na kanuni za ligi.

Geofrey Nyange - Makamu wa Rais wa Simba