Mwamuzi Martin Saanya (Katikati) katika mechi ya Simba na Yanga Oktoba Mosi mwaka huu
Mwenyekiti wa kamati hiyo Salum Umande amesema jambo hilo haliwezekani kwa kuwa ni kinyume cha kanuni za uendeshaji wa ligi, pia ni kinyume cha sheria na taratibu za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na kuwataka Simba wasubiri hadi kanuni zitakapobadilika.
Amesema katika kanuni za ligi zilizopitishwa na vilabu msimu huu zinaeleza kuwa waamuzi watakaochezesha mechi zote za ligi watatakiwa kutoka Tanzania Bara. "Yaani hatuwezi kuchukua mwamuzi hata kutoka Zanzibar, tutakuwa tunafanya kinyume na kanuni". Amesisitiza.
Salum Umande - Mwenyekiti Kamati ya Waamuzi
Kuhusu FIFA, Umande amesema kuwa FIFA hairuhusu timu kuhusika katika ushawishi wa kupanga mwamuzi, kitendo ambacho hutafsiriwa kama rushwa.
Akizungumzia hatua ambazo Simba wamesema wataichukua ya kutopeleka timu uwanjani katika mechi yao ya marudiano dhidi ya Yanga, Umande amesema kanuni za ligi ziko wazi na mamlaka husika itachukua uamuzi stahiki kwa timu ambayo haitatokea uwanjani siku ya mchezo.
Haji Manara
Klabu ya Simba siku ya jana kupitia kwa msemaji wake Haji Manara ilitoa malalamiko yake juu ya kutosikilizwa kwa madai yao mbalimbali ambayo wamekuwa wakiyawasilisha TFF, likiwemo suala la waamuzi ambao wamechezesha mechi mbili zilizopita dhidi ya Yanga, huku ikitaka mechi zijazo zipangiwe waamuzi kutoka nje ya Tanzania ili kujenga imani.