Friday , 11th Sep , 2015

Simba SC itamkosa mshambuliaji wake hatari, Ibrahim Hajib katika mchezo wake wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara kesho dhidi ya African Sports uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

Hajib, mkali wa mabao wa Msimbazi, pamoja na viungo Jonas Mkude na Abdi Banda wote ni majeruhi na hawajasafiri na timu Tanga kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali.

Katika taarifa yake Nahodha wa timu hiyo Mussa Hassan 'Mgosi' amesema, wamefika salama Tanga na jana jioni walifanya mazoezi mepesi kwa ajili ya kuendelea kujiweka 'fiti' kuwavaa African Sports hapo kesho.

Mgosi amesema wameimarika na wapo tayari kusaka pointi tatu katika mchezo huo wa kwanza ili kujitengenezea mazingira ya ushindi kwenye mchezo unaofuata.

Mshambuliaji huyo aliyerejea Simba akitokea Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro msimu huu amesema mazoezi waliyofanya kujiandaa na ligi hiyo yalikuwa magumu na lengo lake ni kuhakikisha 'wanaiva' na kupata ushindi katika kila mechi watakayocheza.