
Waziri wa wizara ya habari, utamaduni michezo na sanaa Nape Nnauye akizungumza katika moja ya mikutano na waandishi wa habari.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam waziri wa wizara hiyo Nape Nnauye amesema yeye na viongozi wa klabu, shirikisho la soka nchini TFF na mkuu wa mkoa wa Shinyanga wameamua kufikia maamuzi ya kuiacha klabu kwa wamiliki halali ambao wataiongoza kwa kufuata misingi ya katiba yao.
Nnauye ameongeza kuwa wizara yake ilikaa kikao kuangalia kwa kina mgogoro huo na kubaini unasababishwa na kamati iliyoundwa chini ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Ally Lufunga ambayo inashinikiza kufanyika kwa uchaguzi wa viongozi wapya.
Alisema kuwa baada ya kubaini hilo wakaona njia ya kuondoa mgogoro huo ni kuitimua kamati hiyo na kuiacha timu chini ya uongozi uliopo sasa chini ya Mwenyekiti wake Amani Vicent.
Hata hivyo Nnauye amesema uongozi unarudishiwa mamlaka yake na kusimamia mambo yao wakati huohuo mdhamini ambaye ni kampuni ya ACACIA ahakikishe pesa yake inatumika vizuri ndani ya klabu na uongozi uhakikishe wanaajiri wataalamu wazuri wasimamie fedha watakazopewa.