Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wakifanya mazungumzo na shabiki mmoja wa soka baada ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa malimu nyerere DSM, Mwezi Machi mwaka huu.
Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wametua Dar es Salaam leo (Mei 17 mwaka huu) mchana, na kujiunga moja kwa moja kwenye kambi ya Taifa Stars kwa ajili ya michuano ya Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza ya michuano hiyo itafanyika kesho (Mei 18 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Washambuliaji hao wa Taifa Stars wamewasili saa 7.25 mchana kwa ndege ya Ethiopian Airlines wakitokea Khartoum, Sudan ambapo jana (Mei 16 mwaka huu) timu yao ya TP Mazembe ilicheza mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Hilal ya huko.
Kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij amesema kikosi chake kipo tayari kwa ajili ya mechi hiyo, kwani kimepata mechi za kirafiki na mazoezi ya kutosha kwenye kambi iliyoanzia Tukuyu mkoani Mbeya ambapo kulikuwa na utulivu mkubwa.
Naye Kocha Msaidizi wa Zimbabwe, Kalisto Pasuwa amesema hawaifahamu vizuri Taifa Stars lakini wamekuja kwenye mechi hiyo itakayoanza saa 10 jioni kwa ajili ya kushinda, na kuwataka washabiki wajitokeze kwa wingi kuona kiwango cha timu yake.
Milango kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi kutoka Ghana wakiongozwa na Joseph Odartei Lamptey itakuwa wazi kuanzia saa 6 kamili mchana, na tiketi zitapatikana katika magari maalumu uwanjani hapo.
Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, kijani na bluu, sh. 10,000 kwa VIP C na B, na sh. 20,000 kwa VIP A.