Monday , 22nd Oct , 2018

Mkurugenzi wa Singida United, Festo Sanga ameweka wazi juu ya sababu inayopelekea wachezaji wake kuondoka katika klabu hiyo tofauti na ukata wa fedha pekee kama inavyotajwa.

Wachezaji wa Singida United

Singida United imeondokewa na wachezaji wake muhimu tangu mwanzoni mwa msimu huu wakiwemo, Tafadzwa Kutinyu, Miraji Adam pamoja Manyika Peter Jr ambao tetesi zinaeleza kuwa wameachana na klabu hiyo kisa kutolipwa pesa zao. 

Akizungumza na www.eatv.tv, Festo Sanga amesema, "Kwanza kabisa naomba watu watambue kuwa Singida United haijatetereka katika hilo na sababu ya wachezaji hao kuondoka sio ukata wa fedha, hapana".

"Kikosi chetu kina wachezaji 35, sasa katika wachezaji hao,  wachezaji wanaoanza katika kikosi ni 18, kwahiyo wengine wanatakiwa wafanye kazi kubwa ya kumshawishi kocha ili kuingia kwenye kikisi cha kwanza. Sasa mchezaji anapokaa muda mrefu hajacheza anaona bora atafute changamoto nyingine ", ameongeza.

Akizungumzia kuondoka kwa mchezaji Miraji Adam, Festo Sanga amesema kuwa mchezaji huyo ameondoka baada ya kuwaandikia barua viongozi wa klabu hiyo akiomba kuondoka, tofauti na sababu ya ukata inayozungumzwa.

Aidha amekiri kuwa klabu hiyo imetetereka msimu huu kutokana na ukata ambao inapitia huku akiitaja sababu kubwa ya ukata huo ni kutokana na ligi kutokuwa na mdhamini mkuu pamoja na mdhamini wa klabu hiyo kujitoa.