Tuesday , 8th Nov , 2016

Klabu ya Ruvu Shooting inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara imeahidi kuizawadia Yanga pointi 3 katika mchezo uliopangwa kupigwa kesho katika dimba la Uhuru Dar es Salaam.

 

Kauli hiyo imetolewa na msemaji wa Ruvu Shooting Massau Bwire, wakati akilalamikia mabadiliko ya ratiba yaliyofanywa na Bodi ya Ligi, ambapo awali mechi hiyo ilikuwa imepangwa kuchezwa kesho kutwa Alhamis, kabla ya kubadilishwa tena na kuwa Jumatano.

Massau amesema kuwa kwa hali halisi ilivyo, wachezaji wa Ruvu Shooting ambao wako safarini kutokea Kagera watafika Dar es Salaam wakiwa wamechoka kwa kuwa wanatumia usafiri wa barabara, hivyo hawatapata muda wa kupumzika, jambo litakalowasababisha wasicheze soka la ushindani siku ya kesho.

"Tuliomba mechi yetu ichezwe Novemba 11 ili tupate muda wa safari kutoka Bukoba na wa kupumzika, wakatukubalia, lakini baadaye wakatuletea mabadiliko kuwa ni lazima mechi yetu ifanyike Novemba 10 kwa kuwa kuna mechi ya timu ya taifa, tukaona haina shida kwakuwa tungepata siku mbili za kujiandaa, lakini cha kushangaza jana Jumatatu tunaletewa barua kuwa mechi yetu na Yanga itafanyika Jumatano Novemba 9, hiyo siyo haki, kama watalazimisha basi wajue tunakwenda kucheza soka lisilo la ushindani, tunakwenda kuwapa Yanga pointi 3 za bure" Amesema Massau Bwire.

Ruvu Shooting imecheza na Kagera Sugar siku ya Jumapili katika dimba la Kaitaba Bukoba na kupoteza kwa kuchapwa mabao 3-1, huku Yanga ikicheza pia siku hiyo mkoani Mbeya na kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya prisons.

Kwa mujibu wa Bodi ya Ligi, ratiba imelazimika kupanguliwa ambapo mechi hizo zilizokuwa zimepangwa kupigwa siku ya Alhamis Novemba 10, zimerudishwa nyuma kwa siku moja ili kutoa nafasi ya maandalizi ya mechi ya kirafiki ya kimataifa kati ya Zimbabwe na Taifa Stars, huku ikisisitiza kuwa ratiba hiyo imezingatia vigezo vyote na haiwezi kubadilika tena.

Timu nyingine iliyolalamikia mabadiliko hayo ya ratiba ni Simba ambayo kesho inakipiga na Prisons Jijini Mbeya.