Cristiano Ronaldo akiruka juu kuifungia Ureno goli la kwanza.
Ureno imekuwa nchi ya kwanza kuingia fainali ya michuano ya Euro baada ya kuzima ndoto za Wales kwa kuichapa magoli 2 - 0 katika mechi ya nusu fainali mjini Lyon nchini Ufaransa.
Kipigo hicho kwa vijana wa Wales wanaonolewa na kocha Chris Coleman kimefuta kabisa ndoto ya nchi hyio kutaka kuweka Historia mpya ya nchini hiyo katika soka katika michuano mikubwa tangu walipofanya hivyo mnamo mwaka 1958 na walikuwa na matumaini ya kufikia azma hiyo hasa baada ya awali kuichapa timu ngumu ya Ubelgiji kwa jumla ya mabao 3-1 katika robo fainali.
Mshambuliaji wa Ureno Cristiano Ronaldo ameendelea kuwa mwiba kwa wapinzani kwenye mashindano hayo baada ya kupachika goli katika kipindi cha pili kabla mshambuliaji wa zamani Manchester United Luis Nani kupigilia msumari wa moto kwenye kidonda kwa kupachika goli la pili dakika tatu baadaye.
Ronaldo alifunga goli la kwanza katika dakika ya 50 na kusababisha la pili lililofungwa na Louis Nani na kuzima ndoto za Wales iliyokuwa ikiongozwa na Gareth Bale anayekipiga timu moja ya Real Madrid na Ronaldo.
Awali, kulikuwa na ubishi, nani kati ya Ronaldo na Bale atatinga fainali, ingawa Bale alionyesha kiwango bora kabisa lakini sasa jibu liko hadharani.
Hadi inatinga nusu fainali, Ureno haikuwa imeshinda hata mechi moja ndani ya dakika 90. Pia ilivuka hatua ya makundi ikiwa best looser, lakini jana usiku imeshinda kwa mara ya kwanza ndani ya dakika 90 na kufanikiwa kusonga fainali.
Kwa matokeo hayo Ureno sasa itakutana katika fainali na mmoja wa mshindi wa nusu fainali itakayopigwa Julai 7 mwaka huu baina ya wenyeji Ufaransa au Ujerumani.
Wakati huo huo pamoja na kuiongoza Ureno kushinda magoli 2-0 dhidi ya Wales na kutinga fainali ya Euro 2016, Cristiano Ronaldo ameweka rekodi ya kufunga goli lake la 9 katika michuano ya Euro.
Kwa goli hilo la 9, maana yake amemfikia mfungaji bora wa miaka yote wa michuano ya Euro, Michell Platini wa Ufaransa.
Ronaldo amebakiza mchezo mmoja dhidi ya mshindi kati ya nusu fainali ya pili baina ya Ujerumani na wenyeji Ufaransa na kama Ronaldo atafanikwia kupachika goli katika mchezo wa fainali hiyo itakayopigwa Julai 10 mwaka huu basi atakuwa ameweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa michuano ya Euro.