Wachezaji wa mchezo wa RollBall wakifanya mazoezi.
Rais wa chama cha mchezo wa RollBall Tanzania TRBA, Noel Kihunsi ametoa wito kwa makampuni na wadau wote hapa nchini kushirikiana na chama hicho katika mchakato wa kuendeleza na kukuza mchezo huo hapa nchini kama ilivyo kwa wenzetu Kenya.
Kihunsi ambaye pia ni kocha wa mchezo huo amesema Kenya kwa jinsi ilivyopiga hatua kwa kasi katika mchezo huo hasa kutokana na kuungwa mkono moja kwa moja na Serikali ya nchini hiyo ni wazi imekuwa ni nchi ya mfano na kimsingi Tanzania nayo inapaswa kuiga mwenendo huo ili kufanikiwa kupitia mchezo huo ambao sasa umeanza kuenea maeneo mengi hapa nchini.
Kihunsi amesema mchezo huo pamoja na kuwa haujaenea maeneo mengi nchini lakini umekuwa ni moja ya michezo ambayo itailetea sifa kwa haraka nchini na pia tayari umekuwa na rekodi ya kutosha kwa muda mfupi kwani tayari tangu kuasisiwa kwa mchezo huo hapa nchini miaka michache iliyopita Tanzania imeshashiriki mara mbili michuano ya dunia ikishiriki kwa mara ya kwanza michuano iliyofanyika nchini India ikishirikisha mataifa 17 wanachama wa mchezo huo na kushika nafasi ya tano.
Akimalizia Kihunsi amesema kuungwa mkono na makampuni, wadau na Serikali itakuwa fursa kwa mchezo huo ambao bado haujaenea kwa kasi katika maeneo mengi nchini kuanza kusambaa na hatimaye kuongezeka kwa washiriki na vilabu ambavyo baadaye vitashindanishwa na kupata kikosi bora cha Taifa kitakachotokana na wachezaji ambao wameshindana kuanzia ngazi za chini hadi taifa.