kocha wa Taifa Stars, Mart Nooij
Kocha mpya wa Taifa Stars, Mart Nooij ameongeza wachezaji tisa katika kikosi hicho kinachojiandaa kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Malawi (The Flames) itakayochezwa Mei 4 mwaka huu katika Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Wachezaji walioongezwa ni Edward Charles Manyama (JKT Ruvu), Elias Maguli (Ruvu Shooting), Hassan Dilunga (Yanga), Hussein Javu (Yanga), John Bocco (Azam), Kelvin Friday (Azam), Oscar Joshua (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe (AC Cannes, Ufaransa).
Naye beki Kelvin Yondani wa Yanga ambaye aliitwa awali ameondolewa katika kikosi hicho kwa vile ameshindwa kuripoti kambini.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Pemium Lager inaingia kambini kesho (Aprili 28 mwaka huu) jijini Mbeya kujiandaa kwa mechi dhidi ya Malawi.
Wakati huo huo, Tanzania (Taifa Stars) imepangiwa kucheza na Zimbabwe katika raundi ya pili ya mechi za mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika (AFCON) zitakazofanyika mwakani nchini Morocco.
Stars itaanzia nyumbani ambapo mechi ya kwanza itachezwa kati ya Mei 16 na 18 wakati ile ya marudiano itachezwa Harare kati ya Mei 30 na Juni 1 mwaka huu.