Manchester United imemteua kiungo wa zamani wa klabu hiyo Nick Butt kuwa kocha mkuu wa timu ya vijana ya klabu hiyo.
Butt, mwenye umri wa miaka 41, alipitia timu za vijana za Unitedna alicheza kwenye klabu hiyo katika kipindi cha kuanzia 1992 na 2012 akicheza jumla ya michezo 387.
Butt,alifanya kazi kama kocha wa kikosi cha akiba na kocha wa timu ya umri wa miaka 19,tangu arejee klabuni hapo mwaka 2012.
Makamu Mtendaji Mkuu wa Manchester United Ed Woodward alisema "Nick ana urithi na utamaduni wa klabu ndani ya damu yake. Ni chaguo halisi".
Kwa upande wake, Butt alisema "Kama mtu aliyejifunza vitu kwenye mfumo wa soka la vijana la United ni heshima kubwa kupewa nafasi kuongoza shule ya vijana na kuendeleza maadili yake na mitazamo katika kujenga kizazi kijacho cha wachezaji wa Manchester United".
Butt alishinda vikombe sita vya ligi kuu ya soka nchini Uingereza katika muda wake ndani ya Old Trafford na kucheza mara 36 kwenye kikosi cha timu ya taifa ya soka ya Uingereza.
Pia aliyeteuliwa kama msaidizi wa aliyekuwa kocha wa muda wa Manchester United Ryan Giggs kwa ajili ya kusimamia mechi nne za mwisho za msimu wa 2013-2014, baada ya kufukuzwa kazi David Moyes.






