Saturday , 29th Jul , 2017

Baada ya tambo za manahodha wa timu nne zinazochuana kwenye hatua ya nusu fainali ya michuano ya Sprite B Ball Kings, leo itajulikana ni timu gani itakayofuzu au kujiweka katika mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya fainali ya michuano hiyo.

Ni kwenye michezo itakayochezwa leo kwenye viwanja vya Don Bosco Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuibuka na ushindi kwenye nusu fainali ya kwanza iliyochezwa Jumamosi iliyopita, timu ya Kurasini Heats leo itajaribu kusaka ushindi  utakaoipeleka kwenye moja ya fainali itakapokabiliana tena na TMT.

Nahodha wa Kurasini Heats, Rajab Hamis, alisema kuwa wataingia uwanjani leo kusaka ushindi wa pili utakaowapeleka fainali.

“Tutaingia uwanjani kwa lengo moja tu la ushindi, tumewaona wapinzani wetu wana udhahifu sehemu gani, tutatumia udhaifu huo,” alisema Hamis.

Aidha, nahodha wa TMT, Is-haka Masoud, alisema hawatarajii kurudia tena makosa waliyoyafanya kwenye mchezo uliopita. Mchezo huo kati ya Kurasini Heats dhidi ya TMT utakuwa wa kwanza ambao utaanza saa 8:00 mchana na utafuatiwa na mchezo kati ya ‘wababe’ Mchenga dhidi ya Flying Dribblers.

Katika nusu fainali ya kwanza iliyochezwa Jumamosi, Mchenga ilitoa kipigo cha mbwa mwizi cha pointi 116-69, endapo Kurasini Heats na Mchenga zitashinda michezo ya leo moja kwa moja zitakuwa zimeingia kwenye hatua ya fainali na kama zitapoteza zitalazimika kucheza nusu fainali ya tatu.