Mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga akishangilia moja ya bao aliloofungia klabu yake bao kwenye mechi za ligi kuu ya soka Tanzania bara.
Bao pekee la mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma mnamo dakika ya 17 limeipa mwanzo mzuri klabu ya Yanga katika mchezo wa kwanza Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuwafunga wenyeji wao Cercle de Joachim 1-0 mchana wa leo huko nchini Mauritius.
Kwa ushindi huo, Yanga SC sasa watakuwa na kazi nyepesi katika mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo mjini Dar es Salaam, wakihitaji hata sare ili kusonga mbele, ambako watakutana na mshindi kati ya APR ya Rwanda na Mbabane Swallows ya Swaziland.
Baada ya mchezo huo, Yanga inatarajiwa kurejea nchini na kuelekea kisiwani Pemba kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wa ligi kuu ya sokaTanzania Bara dhidi ya mahasimu wao klabu ya Simba Jumamosi ya wiki ijayo katika uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Nao wawakilishi wengine wa Tanzania kutoka visiwani Zanzibar Mafunzo wamenyukwa mabao 3-0 wakiwa nyumbani na As Vita ya Congo DR .






