Kocha Mzambia Patrick Phiri akisaini mkataba wa mwaka mmoja mbele ya mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba Colin Firsch
Klabu ya soka ya Simba imeingia mkataba wa mwaka mmoja na kocha Mzambia Patrick Phiri kocha ambaye kwa awamu tofauti alizowahi kukinoa kikosi cha timu hiyo alishinda mataji mawili ya Ligi Kuu, misimu ya 2004/2005 na rekodi bora kabisa ya kukumbukwa na wanasimba ni ya mwaka 2009/2010 kwa timu hiyo kushinda ubingwa bila kupoteza mchezo hata mmoja na pia alishinda Makombe ya Tusker mwaka 2005 nchini Tanzania na baadaye nchini Kenya.
Lakini pia Phiri anakubalika kwa namna alivyoweza kuiongoza Simba SC kuwatambia watani wa jadi, Yanga SC kwa kipindi chote ambacho alikuwa akiinoa timu hiyo kwa nyakati tofauti jambo ambalo linamfanya awe kocha mwenye heshima ya kipekee kwa wana msimbazi kote nchini
Katika awamu zote tatu alizofundisha Simba SC hapo kabla, kocha Phiri hajawahi kufukuzwa- kwani amekuwa akiondoka mwenyewe kwa sababu mbalimbali
Kihistoria kocha Phiri ni kocha mwenye mafanikio tangu anacheza soka katika klabu za Rokana United (sasa Nkana F.C.) na Red Arrows zote za nyumbani kwao, Zambia kama mshambuliaji
Alikuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Zambia kilichocheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1978 na 1982, kabla ya kuiwezesha Chipolopolo kufuzu kwa AFCON ya mwaka 2008 nchini Ghana
Akiwa kocha, Phiri pia aliiongoza timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Zambia kucheza Fainali za kwanza kabisa za Kombe la Dunia nchini Nigeria mwaka 1997 kabla ya kushinda tuzo ya kocha bora wa mwaka nchini mwake mwaka 1999
Simba SC Jumapili ilivunja mkataba na Mcroatia, Zdravko Logarusic ikiwa ni siku moja tu baada ya timu hiyo kufungwa mabao 3-0 na ZESCO ya Zambia katika mchezo wa kirafiki Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Loga ambaye aliongezewa Mkataba wa mwaka mmoja mwezi uliopita- inadaiwa amefukuzwa kwa sababu za kutotii miiko na maadili ya klabu na Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva alisema kwamba uamuzi huo umekuja baada ya kumvumilia kwa kiasi cha kutosha.