Soka la Ufukweni
Michuano ya mpira wa miguu ya ufukweni (Beach Soccer) inazinduliwa rasmi keshokutwa (Aprili 20 mwaka huu) kwenye ufukwe wa Escape One uliopo Mikocheni, Dar es Salaam na kushirikisha timu 13.
Uzinduzi huo utaanza saa 5 asubuhi na mechi zitachezwa hadi saa 11 jioni. Michuano hiyo inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini inashirikisha timu 13 kutoka vyuo mbalimbali vya jijini Dar es Salaam.
Vyuo hivyo ni Chuo Kikuu cha Ardhi (AU), Chuo Kikuu cha St. Joseph Tanzania (SJUIT), Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (TUDARCO), Chuo cha Ustawi wa Jamii (ISW), Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Vingine ni Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo cha Utawala wa Kodi (ITA) na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT).
Michuano hiyo itakuwa inachezwa Jumamosi na Jumapili kwenye fukwe za Escape One na Gorilla Beach iliyopo Kigamboni, Dar es Salaam.