Friday , 10th Aug , 2018

Klabu ya Barcelona imempa rasmi Lionel Messi majukumu ya kuiongoza klabu hiyo ndani ya uwanja kama nahodha kuanzia msimu huu, akiirithi nafasi ya Andres Iniesta aliyejiunga na ligi ya Japan.

Lionel Messi akivalishwa kitambaa cha unahodha na Andres Iniesta katika moja ya mchezo wa klabu bingwa Ulaya.

Messi aliyejiunga na klabu hiyo tangu mwaka 2001 amecheza michezo 669 na kufunga mabao 552 yanayomfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa klabu hiyo.

Amekuwa pia nahodha wa timu ya taifa ya Argentina tangu mwaka 2011 akirithi nafasi ya Alejandro Sabella.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa katika mtandao wa kijamii wa Twitter wa klabu hiyo, Messi atasaidiwa na wachezaji watatu, Sergio Busquets, Gerard Pique na Sergi Roberto katika uongozi huo huku wachezaji wote wakiwa ni zao la kituo cha kukuza vipaji cha klabu hiyo cha La Masia.

Kwenye michezo yote ya maandalizi ya msimu mpya wa 2018/19 nchini Marekani, Barcelona ilikuwa chini ya nahodha, Sergi Roberto baada ya Lionel Messi kuwa katika likizo yake kufuatia kumalizika kwa michuano ya kombe la Dunia nchini Urusi.