Pichani ni Nembo ama Logo ya Liki kuu.
Ligi kuu ya soka Tanzania bara mzunguko wa hatua ya lala salama unataraji kuendelea tena mwishoni mwa juma hili katika viwanja mbalimbali kote nchini kwa miamba ya ligi hiyo kusaka alama tatu muhimu katika michezo yao.
Ratiba ya ligi hiyo ambayo mpaka sasa mabingwa watetezi Yanga ndiyo vinara wa ligi hiyo wakiwa na alama 62 kwa michezo 25 inaonyesha kuwa jumamosi kutapigwa mitanange mitano [mechi tano] ambapo jumapili kukipigwa mtanange mmoja baina ya wenyeji Simba na Azam fc.
Michezo hiyo mitano ya jumamosi hii kwa mujibu wa ratiba ni kama ifuatavyo-:
Vinara wa ligi hiyo VPL timu ya soka ya Yanga wao watakuwa ugenini jijini Mwanza kupambana na timu isiyotabirika ya Wanakishamapanda Toto Africans katika mchezo ambao unatarajiwa kuwa wa vuta nikuvute huku Yanga ikizihitaji alama tatu muhimu ili iendelee na mbio za kutetea ubingwa huo.
Pamoja na umuhimu wa mchezo huo kwa Yanga na utabiri wa wachambuzi wa soka kwamba uhenda mchezo huo ukatoa matokeo ambayo hayakutarajiwa hasa kutokana na timu ya Toto kuwa ngumu hasa ikicheza nyumbani lakini baadhi ya wachambuzi wanaona mchezo huo utakuwa mwepesi kwa Yanga kwa mambo makuu mawili
-: kwanza ni uswahiba wa timu hizo mbili ambazo zinaudugu wa hiari zikishabihiana hata kwa rangi ya jezi zao lakini kubwa la pili ni kuwa baada ya Watoto hao wa Mwanza kuibuka na ushidi dhidi ya Simba nakujihakikishia kubaki daraja basi wadau wameona kuwa nayo inaweza kuwa sababu ya wanakishamapanda hao kucheza kinazi na kuwapa nafasi Yanga kupata matokeo katika mchezo huo.
Mechi nyingine ni kule katika dimba la Mkwakwani jijini Tanga ambako kutakuwa na mechi ya watani maarufu kama Tanga Dabi ambayo itawakutanisha wenyeji wa siku hiyo Wanakimanumanu African Sports ambao watawavaa Wagosi wa Kaya Coastal Union katika mchezo mgumu mno ambao utaamua ama kutoa mwanga wa nani anazama ama kuanza kujinasua kutokana na timu zote hizo kuwa mkiani mwa ligi hiyo.
Dabi nyingine itakuwa kule Shinyanga wakati wachimba madini ama almas wa Mwadui fc watakapowaalika wapinzania wao wa jadi Stand United katika mchezo maarufu kama Shinyanga Dabi mchezo utakaopigwa katika Dimba la Mwadui Complex.
Huko Katika dimba la Manungu Tuliani Mjini Morogoro wenyeji wakata miwa wa huko Mtibwa Sugar watawaalika katika mashamba hayo ya miwa timu ya wagonga nyundo wa jiji la Mbeya timu ya Mbeya City na mchezo wa mwisho hiyo kesho ni baina ya wenyeji maafande wa Magereza Tanzania Prisons ya jijini Mbeya watakaowaalika maafande wa jeshi la kujenga taifa JKT Ruvu katika mchezo utakaochukuwa nafasi katika dimba la Sokoine jijini humo.
Na jumapili ni zamu ya wapinzania wa mji wa Dar es Salaam Simba na Azam ambapo mchezo huo wa Ligi Kuu Bara ni muhimu zaidi na maradufu kwa Simba, Kwa kuwa kama itapoteza mechi hiyo, itakuwa imejiondoa rasmi katika mbio za ubingwa.
Simba ina pointi 57 katika nafasi ya tatu, Azam FC ina 58 katika nafasi ya pili. Simba inahitaji kushinda ili kuendelea kuwa katika mbio hizo.
Kama itaishinda Azam FC itakuwa imefikisha pointi 60 na kupanda hadi nafasi ya pili. Kwa kuwa Yanga ndiyo vinara na tayari wana pointi 62 kabla ya kuivaa Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza,hapo kesho.