Wednesday , 24th Jun , 2015

Timu ya Coastal Union,Wagosi wa Kaya ya jijini Tanga imeingia mkataba wa miaka miwili na aliyekuwa Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Jackson Mayanja ambaye ni raia wa Uganda kuifundisha Coastal katika msimu ujao wa Ligi kuu soka Tanzania Bara.

Kocha Mkuu wa Coastal Union, Jackson Mayanja

Katika taarifa yake, Afisa habari wa timu hiyo, Oscar Assenga amesema, kutokana na umahiri aliokuwa nao kocha huyo wanaimani kubwa ataipa mafanikio timu hiyo hasa katika harakati za kuhakikisha inafanya vizuri ligi kuu msimu ujao.

Assenga amesema, uwezo wa kocha huyo utawapa matumaini makubwa ya mafanikio kutokana na uwezo mzuri wa kufundisha na kuzipa mafanikio timu hivyo atakuwa chachu katika maendeleo.

Mayanja ambaye aliwahi kuzifundisha timu za soka Kiyovu FC ya Rwanda,Timu ya Mamlaka ya Mapato nchini Uganda (URA),Vipers FC ya Bunamwaya na KCC ya Uganda amesema kutua kwenye timu hiyo kumpa faraja kubwa hivyo atahakikisha anatoa mchango wake kwenye kuipa mafanikio.

Mayanja amesema,mipango yake mikubwa ni kuhakikisha timu hiyo inaonekana vizuri katika michuano ya ligi kuu msimu ujao ikiwemo kubadili aina ya mchezo wa timu hiyo ili iweze kupata mafanikio kwa kuweka umoja baina ya wachezaji mashabiki, wanachama na wapenzi.

Mayanja amesema kama mshikamano baina ya wapenzi,wanachama na viongozi utakuwepo utasaidia kuiwezesha timu hiyo kuchukua Ubingwa wa ligi kuu msimu ujao kwani dhamira yake ni kutaka kuona timu hiyo inafanya vizuri kwenye medani za kitaifa na kimataifa.