Saturday , 26th Dec , 2015

Baada ya kuwindana kwa muda mrefu mabondia wa Tanzania, Thomas Mashali wa Dar es Salaam na Francis Cheka wa Morogoro jana usiku walishuka ulingoni katika uwanja wa jamhuri mjini Morogoro kukata mzizi wa fitina wa nani zaidi baina ya wawili hao.

Mabondia Thomas Mashali kushoto na Francis Cheka wakiwa tayari kwaaajili mpambano wao hapo jana.

Bondia mtanzania Thomas Mashali wa Dar es Salaam amefanikiwa kulipa kisasi mara baada ya jana usiku kufanikiwa kuibuka na ushindi wa pointi dhidi ya mpinzani wake mtanzania Francis Cheka [SMG] katika mpambano mkali wa raundi 12 kuwania ubingwa wa Tanzania uzito wa kati kilo 76.

Thomas Mashali ambaye mnamo mwaka 2013 alipigwa Knock-Out ya raundi ya 10 na Cheka jana tangu awali alionekana amefika mjini Morogoro kusaka ushindi mara baada ya kuanza mpambano huo kwa kasi huku akitumia akili nyingi na kutawala pambano hilo kwa kiasi kikubwa.

Mabondia hao waliendelea kushambuliana kwa zamu katika raundi zote hadi mpambano unamalizika mwana Dar es Salam Thomas Mashali maarufu kama Simba asiyefugika aliibuka na ushindi wa point toka kwa maamuzi ya majaji wawili kati ya watatu na hivyo kufuta uteja kwa bondia mtoto wa Morogoro Francis Cheka maarufu kama [SMG] katika mpambano huo mkali uliopigwa katika dimba la Jamhuli mjini Morogoro.

Point za majaji zilikuwa kama ifuatavyo:
Mashali alipata Jumla ya point 287 (94, 96, 97) dhidi ya point 282 (96, 93, 93) alizopata Cheka.