
Simba na Azam katika mchezo wa mzunguko wa kwanza
Kuelekea katika mchezo huo, manahodha wa Azam FC, John Bocco ‘Adebayor’ na Shomari Kapombe, wamewaahidi mashabiki kupambana ili kuweza kuibuka na pointi zote tatu dhidi ya wapinzani wao hao.
Bocco amesema mchezo huo hautakuwa rahisi lakini watajituma na kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
“Tukikutana na Simba tunakuwa tunacheza mpira wa kujuana na pia wa kuogopana, lakini naamini ni mechi ngumu, watakuwa na mipango yao na sisi tutajipanga kwa upande wetu, naamini tutajituma na tutaweza kupata ushindi,” amesema Bocco.
Bocco ataingia kwenye mchezo huo akiwa na rekodi ya aina yake ya kuifunga mabao mengi Simba akiwa tayari ameshaziona nyavu zao mara 18 katika mechi za mashindano mbalimbali.
Kapombe ambaye ni mmoja wa manahodha wasaidizi wa Azam FC, naye amesema kuwa wanaendelea kujipanga vizuri na kufanya maandalizi kuelekea mchezo huo ili kupata ushindi.
Shomari Kapombe
“Jumamosi tuna mechi kubwa na mechi ngumu kwa sababu Simba hivi sasa ndio vinara wa ligi, ni timu nzuri tumeshakutana nayo Zanzibar tumeweza kupata ushindi, hivi sasa tumejipanga vizuri na tunaendelea kufanya maandalizi ili tuweze kupata ushindi kama tulivyofanya mechi iliyopita,” amesema Kapombe.
Timu hizo zinakutana wakati Azam FC ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 31 ikizidiwa pointi 14 na Simba iliyojikusanyia 45 kileleni, Yanga ni ya pili ikiwa na pointi 44 huku Kagera Sugar iliyocheza mchezo mmoja zaidi ikikamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 34.