Saturday , 21st May , 2016

Ikicheza pungufu ikiwa na wachezaji 10 kama ilivyokuwa dhidi ya Bournemouth siku ya jumanne wakati ikimalizia kiporo cha Ligi ya England Manchester United hii imefanya kile walichokuwa wakikisubiri kwa muda mrefu sana mashabiki wa timu hiyo.

Shujaa wa Man United, Jesse Lingard akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la ushindi.

Mashetani wekundu wa Old Trafold timu ya Manchester United wametwaa ubingwa wa Kombe la FA baada ya kuwalaza Crystal Palace kwa mabao 2-1 katika fainali ngumu mno iliyochezewa kwenye uwanja wa kisasa wa Wembley jijini London.

Manchester United ikicheza huku imevalia uzi mweupe katika fainali hiyo ngumu mno iliyodumu kwa dakika 120 iliuanza mchezo huo kwa kasi lakini Crystal Palace ambao walionyesha upinzania wa hali ya juu ndiyo walikuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza likifungwa na mshambuliaji hatari wa timu hiyo Jason Puncheon kunako dakika ya 78 mara baada ya kuingia kipindi cha pili.

Iliwachukua dakika tatu Manchester United kukomboa bao hilo kupitia kwa kiungo Muhispania Juan Mata baada ya kupokea pasi safi ya kifua kutoka kwa kiungo Mbelgiji Marouane Fellaini ambaye alipokea majalo safi kutoka kwa nahodha Wayne Rooney ambaye kabla ya kupiga krosi hiyo aliuchambua ukuta wote wa Crystal Palace na kupiga krosi hiyo iliyokwenda kuzaa bao la kusawazisha la United dakika ya 81.

United ilimaliza pungufu mechi hiyo, baada ya Chris Smalling kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 105 ya dakika 30 za ziada kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea rafu mshambuliaji hatari wa Palace Yannick Bolasie ambaye alikuwa akitaka kuelekea golini kwa United kwa kasi ndipo beki huyo akamshika mguu baada ya awali wote kuanguka chini wakati wakiwania mpira.

Matumaini ya kutwaa ubingwa huo kwa mashetani wekundu na kwa kocha Mdachi Luis Van Gal ambaye kunataarifa zisizo rasmi kuwa huenda mchezo huo ndiyo ulikuwa wa mwisho kwake kutokana na kuwepo na uwezekano mkubwa wakati wowote kuanzia sasa United kumtangaza kocha wa zamani wa Chelsea Mreno Jose Mourinho kuwa kocha mkuu wa timu hiyo, yalifufuka kunako dakika ya 110 baada ya Nyota wa timu hiyo kinda mwenye kasi na ufundi mwingi kiwanjani, Jesse Lingard kuifungia timu yake bao la pili na la ushindi.

Kwa ushindi huo sasa United ambayo tayari ilikuwa na tiketi ya kucheza michuano ya Europa Ligi msimu ujao kutokana na kushika nafasi ya tano katika msimamo wa Ligi kuu ya England EPL inaipa nafasi ya kwenda moja kwa moja katika michuano hiyo timu ya wagonga nyundo wa London West Ham United ambayo ilimaliza katika nafasi ya saba katika msimamo wa ligi ya EPL ikiungana sasa na Southampton iliyomaliza katika nafasi ya sita kucheza michuano hiyo.