
Rais wa Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF Jamal Malinzi ametuma salamu za funga mwaka kwa wadau wa soka nchini katika yale yaliyofanyika kwa mwaka wote wa 2015 kwa ushirikiano wa shirikisho hilo,serikali na Wadau.
Akizungumza jijini Dar es Salaam hii leo Malinzi alianza kwa kumpongeza Rais wa Serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari John Pombe Magufuli na Baraza lake la Mawaziri kwa kuingia madarakani na kupongeza mchakato wa uchaguzi Mkuu hadi kumalizika kwa kwa amani.
Malinzi pia alitoa tathmini nzima ya timu za Taifa za Tanzania zilivyoshiriki katika michuano ya kimataifa,ambapo timu ya Taifa ya wanaume ya Taifa Stars ilifanya vibaya kwa kuondolewa katika michuano ya CHAN chini ya kocha wa Kigeni Mart Nooij,kabla ya kukabidhiwa kocha mzawa Charles Boniface Mkwasa,ambaye aliinua kidogo kiwango cha timu hiyo na kuifunga Malawi na kutoka sare kwenye mechi dhidi ya timu za Algeria na Nigeria.
Pia Malinzi amepongeza ushiriki wa timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania Twiga Stars,iliyokuwa chini kocha Rogasian Kaijage kwenye michuanoya All Africa Games iliyofanyika Congo Brazaville na kutolewa raundi za awali.
Malinzi amesema Shirikisho lina nia njema ya kuendesha soka la nchi lakini inakabiliwa na changamoto za gharama za uendeshaji wa timu za Taifa ni mkubwa ambapo Kwa wastani gharama za kushiriki mkondo mmoja wa mechi ya Kimataifa kwa kucheza nyumbani na ugenini ni takribani shilingi million mia moja (USD 50,000.-), hii inajumuisha gharama za kambi, usafiri kwenda ugenini, posho, nauli na posho za waamuzi na kamisaa, malazi ya waamuzi na kamisaa nk. Kwa kuwa timu yenye udhamini kwa sasa ni timu ya Taifa wanaume tuu hivyo TFF imekuwa inabeba yenyewe gharama nyingine zote kwa timu zote zilizobakia. Imani yetu ni kuwa mwaka 2016 utashuhudia ufadhili unapatikana kwa timu zetu nyingine za Taifa.
Malinzi ameitaka serikali iwekeze zaidi katika michezo kuanzia mwaka ujao ili kurahisisha mazingira ya upatikanaji wa vifaa,miundo mbinu,udhamini na fedha kwa ajili ya kuinua soka la Tanzania.