Rais wa shirikisho la kandanda Tanzania TFF Jamal Malinzi leo amefunga kozi ya waamuzi vijana wasio na beji ya FIFA kutoka nchi mbalimbali barani Afrika lengo likiwa ni kuhakikisha bara la Afrika linapata waamuzi wenye uwezo wa kuchezesha michuano mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla.
Akizungumza mara baada ya hafla ya kukabidhi vyeti kwa waamuzi hao iliyofanyika jijini Dar es Salaam Malinzi amesema ni hatua kubwa kwa Tanzania ambayo imetoa waamuzi wawili ambao nao watakuwa ni chachu kwa wengine ambao hawajashiriki katika kozi hiyo.
Kozi hiyo iliyoanza Septemba 26 na kumalizika leo imeshirikisha waamuzi kutoka mataifa 28 barani Afrika ambao baadaye wataweza kuchezesha mechi na michuano mbalimbali barani Afrika kwa weledi na ubora zaidi.
Kozi hiyo iliendeshwa na wakufunzi kutoka katika nchi za Afrika Kusini, Malawi, Misri na Mauritius ambapo waamuzi chipukizi kutoka Tanzania waliohudhuria ni Abdallah Kambuzi (Shinyanga) na Shomari Lawi (Kigoma).
Lengo la kozi hiyo ni kuwaandaa waamuzi wanaochipukia ili baadaye kuweza kuwa waamuzi wa FIFA ambao watatumika kwa michuano mbalimbali.