Friday , 27th Nov , 2015

Uongozi wa shule ya sekondari ya Makongo umesema, hivi sasa wameamua kutafuta daraja kubwa zaidi katika michezo mbalimbali ili kuweza kuiweka shule hiyo katika nafasi nzuri zaidi katika mashindano ya shule kwa Afrika Mashariki.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Makongo Celestine Mwangasi amesema, vijana wake wamekuwa wakionesha ukomavu na uzoefu katika mashindano suala linalopelekea kutolewa katika michezo hivyo kwa kuwatafutia mashindano ya kirafiki na timu kubwa inawapa uzoefu zaidi.

Mwangasi amesema, wameanza kwa upande wa mpira wa miguu ambapo walianza kwa kucheza na timu zote za ligi daraja la kwanza na wameweza kuzimudu na hivi sasa wameamua kutafuta daraja kubwa zaidi ambapo wanaingia katika mfumo wa ligi kuu ili kuweza kuhimili mikiki mikiki ya timu hizo ambapo leo wameanza na mabingwa watetezi wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara Yanga.

Mwangasi amesema, katika mchezo huo wa kirafiki ambapo vijana wake wamefungwa bao 3-1 imesaidia kuweza kuona vijana wake kiwango walichofikia na mapungufu waliyonayo katika mchezo ili kuweza kuyafanyia kazi na kuweza kusonga mbele zaidi ambapo anaendelea kutafuta timu nyingine za ligi kuu ili kuweza kujipima nazo.