Wednesday , 24th Oct , 2018

Mtanange mkali unatarajiwa kupigwa leo kati ya vinara wa ligi, Azam Fc watakaosafiri kuwafuata JKT Tanzania katika uwanja wao wa nyumbani wa Meja Jenerali Isamuyo.

Wachezaji wa JKT Tanzania (kushoto) na Azam FC (kulia)

JKT Tanzania imekuwa na kiwango bora sana katika mechi zake za nyumbani msimu huu, ikiwa haijapoteza mchezo wowote mpaka sasa katika uwanja huo na viwanja vingine vyote ambavyo imecheza. Ikiwa imecheza jumla ya mechi tisa na kuvuna jumla ya alama 15.

Kwa upande wa Azam Fc, imeshuka dimbani michezo 9 mpaka sasa na kuvuna jumla ya alama 21, ikiongoza ligi kwa tofauti ya alama mbili dhidi ya Yanga inayokamata nafasi ya pili kwa alama 19.

Katika mchezo huo wa leo, JKT Tanzania inatarajia kuzindua kampeni ya kuuza jezi zake kwa mashabiki na wapenzi wa soka kwaajili ya kuiongezea mapato klabu hiyo.

Akizungumzia hatua hiyo, Afisa Habari wa JKT Tanzania, Koplo Jamila Mutabazi amesema kuwa jezi hizo zitauzwa kupitia mawakala wake maalum na kwamba wamejipanga kuzuia aina yoyote ya uuzwaji holela wa jezi hizo.