Tuesday , 30th Oct , 2018

Klabu ya soka ya Simba kupitia kwa Kamati yake ya Uchaguzi imethibitisha kuwa maandalizi ya uchaguzi huo yamekamilika huku ikiwataka wanachama na wagombea kutojihusisha na vitendo vya rushwa.

Mwenyekiti wa kamati hiyo Boniphace Lihamwike.

Akiongea leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti wa kamati hiyo Boniphace Lihamwike, amesema suala la rushwa ni suala la kisheria na kuna chombo ambacho kinahusika hivyo kwa wanachama na wagombea watakaojihusisha navyo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

''Mimi naamini Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ipo kazini muda wote kikubwa  kwa wanachama kuhakikisha hawajihusishi na vitendo hivyo ili wasije wakaingia kwenye mkono wa sheria'', amesema.

Aidha Lihamwike ameweka wazi kuwa ili Mwenyekiti wa Bodi ya klabu hiyo apitishwe ni lazima apate asilimia 50 ya kura zote zitakazopigwa huku wanachama wenye sifa stahiki ikiwemo kadi ambazo zimelipiwa ada ndio watawajibika kuchagua viongozi.

Lihamwike pia amewataka wagombea pamoja na wanachama kuhakikisha wanafanya kampeni za kistaraabu zisizokuwa na vurugu pamoja na rushwa kwa wanachama kwani hatua hiyo itasaidia kupata viongozi wenye sifa.

Katika nafasi ya Uenyekiti amebaki mgombea mmoja ambaye ni Sued Mkwabi baada ya Mtemi Ramadhani kujitoa hivi karibuni. Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Jumamosi Novemba 4, 2018.