Monday , 18th Dec , 2017

Mlinda mlango wa klabu ya Simba Said Mohamed Nduda atamaliza mwaka 2017 akiwa kwenye mazoezi ya “Gym” baada ya kupona majeraha ambayo yamemweka nje tangu msimu huu uanze.

Taarifa ya klabu hiyo imeeleza kuwa mlinda mlango huyo ambaye amesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ameenza mazoezi ya “Gym” chini ya uangalizi wa daktari.

“Kulingana na taarifa ya Daktari wa kikosi cha Simba Dk. Yassin Gembe, Nduda ataendelea kufanya mazoezi haya ya “Gym” chini ya uangalizi wa Daktari kwa mwezi wote huu kabla ya kuanza kufanya mazoezi mepesi uwanjani”, imeeleza taarifa hiyo.

Nduda aliumia mazoezini wakati timu yake ilipokuwa ikijiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga ulioisha kwa Simba kuibuka mabingwa kwa mikwaju ya penalti 5-4.

Huenda atarejea uwanjani kwenye mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania bara baada ya kukosa mechi 11 za mwanzo. Pia ataitumikia klabu hiyo kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Africa.