Kikosi cha timu ya taifa ya soka ya Tanzania bara [Kilimanjaro Stars].
Bara imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji Ethiopia katika mchezo wake wa mwisho wa Kundi A leo Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa. Dakika 45 za kwanza zilimalizika bila ya timu hizo kufungana na kipindi cha pili, Kilimanjaro Stars ilianza kupata bao kupitia kwa Simon Msuva.
Msuva alifunga bao hilo la pili kwake katika mashindano ya mwaka huu kwa kichwa dakika ya 51 akimalizia krosi maridadi ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Hata hivyo, Wahabeshi walifanikiwa kupata bao la kusawazisha baada ya beki Salum Mbonde kujifunga katika harakati za kuokoa mpira uliopigwa na Mohamed Naser dakika za lala salama za mchezo huo.
Kili Stars sasa inamaliza kileleni mwa Kundi A kwa pointi zake saba, ikifuatiwa na Rwanda iliyomaliza na pointi sita, Ethiopia pointi nne, wakati Somalia inaondoka mikono mitupu.
Katika Mchezo wa kwanza leo, bao la dakika ya 70 la Frank Kalanda limeipa Uganda ushindi wa 1-0 dhidi ya Burundi.
Uganda imemaliza kileleni mwa Kundi B kwa pointi zake sita, ikifuatiwa na Kenya pointi nne ambazo zote zinafuzu moja kwa moja Robo Fainali.
Sasa Tanzania Bara [Kilimanjaro Stars] itamenyana tena na Ethiopia katika Robo Fainali Jumatatu, wakati Uganda itacheza na Malawi katika mchezo wa kwanza keshokutwa.
Jumanne Sudan Kusini itacheza tena na Sudan, wakati Rwanda itamenyana na Kenya.
Kikosi cha Tanzania Bara kilikuwa; Aishi Manula, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Salum Mbonde, Kevin Yondan, Himid Mao, Said Ndemla, Jonas Mkude, John Bocco, Elias Maguri na Simon Msuva.