
Salum Mayanga, Kocha wa Mtibwa Sugar
Kocha wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga, amesema atasajili wachezaji wanne kwenye dirisha dogo ili kuziba nafasi ambazo zimeonekana kuwa na mapungufu kwenye mzunguko wa kwanza.
Mayanga amesema kuondoka kwa nyota wanne wa kikosi cha kwanza baada ya ligi ya msimu uliopita kumalizika kumeiyumbisha timu hiyo na kujikuta wakianza vibaya msimu huu.
Kocha huyo wa zamani wa Tanzania Prisons amesema wachezaji wapya waliosajiliwa ni wazuri na wameonyesha kiwango kizuri lakini wamekosa uzoefu kama ilivyo kwa wale walioondoka ambao tayari walikuwa wanaijua vizuri falsafa ya timu na mbinu.
Mayanga, amesema malengo yake kama kocha ni kuiona timu hiyo inatwaa ubingwa msimu huu, lakini kutokana na kuachwa kwa idadi kubwa ya pointi amebadilisha mawazo na kufikiria kumaliza kwenye nafasi tatu za juu na hilo linawezekana kwa sababu ligi bado ni ndefu.
Katika mchezo mwingine uliopigwa leo, Majimaji imepata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwadui katika mchezo uliopigwa Mwadui Complex, Mjini Shinyanga.