Monday , 23rd Feb , 2015

Kesi inayoikabili Shirikisho la Soka Zanzibar ZFA imepigwa tena kalenda na kusogezwa mpaka Aprili tatu mwaka huu.

Akizungumza na East Africa Radio, Katibu Mkuu wa ZFA, Khasim Salum amesema, kesi hiyo dhidi ya ZFA ipo katika mahakama kuu ambapo imefunguliwa na Ally Bakary Ally na imeahirishwa kutokana na mfungua mashtaka kuendelea kukataa kuwa hajafungua kesi hiyo.

Salum amesema kuwa kesi hiyo ya madai ya ubadhirifu wa fedha za kuendesha shughuli za ZFA inayowakabili viongozi wa vyama vya juu imechukua sura mpya kutokana na mfungua mashtaka kukataa na kushtaki kwa kuwa sahihi yake iliyopo mahakamani imegushiwa na suala la kufungua kesi hiyo halipo kwa upande wake.

Salum amesema, mpaka sasa kama shirikisho la soka, halitahusika kusimamia masuala ya soka visiwani humo kutokana na kubanwa na shughuli za mahakamani kwa ajili ya kesi hiyo ambayo mpaka sasa bado hawajajua mwisho wake.
Salum amesema, kesi hiyo itakapomalizika ndipo watajua wanaendelea vipi na mwenendo wa soka visiwani huo.